Mbeya, Akizungumza katika Kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu J.K. Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia nchini (PPPC), Bw. David Kafulila, aliweka wazi changamoto ya umasikini wa kipato na umuhimu wa uwekezaji katika sekta za kijamii na kiuchumi.
Kafulila alibainisha kuwa kumekuwapo na dhana kwamba uchumi wa taifa unaendelea kukua lakini kipato cha wananchi kimekuwa hakiongezeki kwa kasi ile ile. Akifafanua zaidi, alisema kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya umasikini wa kipato na miundombinu duni, hali inayosababisha wananchi kutumia gharama kubwa kufuata huduma muhimu.
“Wakati fulani, wananchi walitumia gharama kubwa kutafuta huduma kuliko gharama ya huduma yenyewe,” alisema Kafulila. “Hii inatokana na ukweli kwamba umasikini au utajiri hupimwa kwa purchasing power – uwezo wa mtu kumudu gharama za huduma.”
Aidha, alisisitiza kuwa ili kupunguza pengo hilo, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa makusudi katika sekta zinazogusa maisha ya watu wengi, zikiwemo kilimo, utalii, burudani, sanaa na michezo. Hatua hizo, alisema, ni sehemu ya kujenga uchumi wa kipato – uchumi unaopunguza gharama kwa wananchi na kuongeza uwezo wao wa kumudu maisha.
Akitoa mfano wa sekta ya afya, Kafulila alisema hatua ya serikali kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 8,700 hadi kufikia zaidi ya 12,800 kwa sasa, ni kielelezo cha jinsi uwekezaji wa moja kwa moja katika huduma unavyopunguza umasikini wa kipato. Kupitia maboresho hayo, wananchi wengi sasa wanapata huduma karibu na makazi yao, hali inayopunguza gharama za usafiri na muda wa kufuata huduma.
Kwa mujibu wa Kafulila, kadri serikali inavyosogeza huduma kwa wananchi, ndivyo inavyoongeza kipato chao kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwani gharama zilizokuwa zikitumika kutafuta huduma sasa zinabaki kwenye mifuko ya wananchi.

