DAVID KAFULILA:NCHI ZOTE DUNIANI ZINAKOPA DENI LA DUNIA NI ZAIDI YA 90% YA UCHUMI WA DUNIA.

Published:

MBEYA, Katika Kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu J.K. Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia nchini (PPPC), Bw. David Kafulila  ametumia jukwaa hilo la Dira2050 kueleza juu ya faida ya kukopa na  hali ya madeni ya kimataifa kwa kuzingatia takwimu za mwaka 2024.

Hadi Oktoba 2024 kwa mujibu wa Kafulila, jumla ya deni la serikali zote duniani lilifikia takribani dola trilioni 102 , wakati Pato la Taifa la dunia (GDP ya dunia) lilikuwa karibu dola za Marekanio trilioni 115. Hii ina maana kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa dunia umefungwa kwenye madeni, hali inayoonesha kumbe hata mataifa makubwa kiuchumi duniani hayakwepi uhalisia wa madeni kama nyenzo yao ya  maendeleo yao.

Katika muktadha huo, Tanzania kuwa na deni linalokadiriwa kufikia asilimia 46 ya Pato la Taifa (GDP) ni hatua inayotazamwa kitaalamu kama salama na yenye kuashiria uimara wa usimamizi wa uchumi. Viwango hivi viko chini ya ukomo wa kimataifa wa deni la serikali unaokubalika (Debt Sustainability Threshold)  na hivyo vinabeba taswira ya matumaini kwa Taifa. Kwa lugha rahisi, hali hii inatupa ujumbe kuwa: Tanzania bado ipo kwenye nafasi nzuri ya kukopa na kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati bila kuhatarisha ustahimilivu wa uchumi wake.

Madeni haya ya dunia yanalenga maendeleo ya watu wao, kwani sehemu kubwa inaelekezwa kwenye miundombinu, huduma za kijamii, na ujenzi wa viwanda, ambavyo vitazaa Pato la baadaye na ajira. Kwa Tanzania Wananchi wanapaswa kuwa na matumaini, kwa sababu kiwango hiki cha deni kinaashiria usalama wa kifedha zao  na kusudi la kulijenga Taifa lao  liwe na uchumi shindani na Jumuishi kwa mujibu wa dira2050.

Kwa hivyo, tafsiri kubwa ya takwimu hizi ni kuwa Tanzania inaendelea kutembea kwenye njia sahihi ya maendeleo, huku ikidumisha nidhamu ya kifedha na kuhakikisha kuwa kila mkopo unaochukuliwa unaakisi faida kwa vizazi vya sasa na vijavyo katika miradi ya kimkakati kama pamoja na barabara, reli, nishati na huduma za kijamii, miradi ambayo faida zake zinawagusa moja kwa moja wananchi kwa kuongeza ajira, kukuza biashara na kuchochea uchumi. Hii ni habari ya matumaini kwa Watanzania wote: deni si mzigo usio na tija, bali ni nyenzo ya maendeleo likitumika kwa nidhamu na malengo sahihi. Tanzania imechagua njia salama ya kukua haraka kiuchumi, njia inayowaweka wananchi katikati ya manufaa ya kila shilingi inayokopwa , kuna msemo wa wahenga unasema “aliyekopa kajenga, aliyekaa kajionea”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img