DKT FRED MSEMWA: MAONO LAZIMA YAWE YA KUKUTISHA KAMA TAIFA TUMEMUA KUWA NA NDOTO KUBWA.

Published:

Mbeya || Akizungumza katika Kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu J.K. Nyerere katika Taaluma za Umajumui wa Afrika, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Katibu Mkuu wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, aliweka bayana kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuibua mabadiliko ya kimsingi katika sekta ya nishati, hususan matumizi ya umeme, kama kichocheo cha ustawi wa taifa kipimo cha ukuaji halisi wa Uchumi.

Fred anasema shabaha ya Matumizi ya umeme kwa mtu mmoja mmoja na umri wa kuishi vinachukuliwa kama kipimo muhimu cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Mwaka 2025, wastani wa matumizi ya umeme kwa mtu mmoja unakadiriwa kuwa takriban 170 kWh kwa mwaka, kiwango kinachowakilisha matumizi ya msingi kwa kaya zenye vifaa vya kawaida kama taa, redio, na simu. Ongezeko hili linatokana na juhudi za serikali kupanua upatikanaji wa umeme vijijini na mijini kupitia miradi ya gridi ya taifa na mini grid.

Ifikapo mwaka 2030, matumizi ya mtu mmoja yanatarajiwa kuongezeka hadi 300–800 kWh kwa mwaka, yakichochewa na upanuzi wa miundombinu ya nishati, ongezeko la matumizi ya vifaa vya umeme majumbani, na kuimarika kwa huduma za kijamii zinazotegemea umeme. Mwaka 2040, kiwango hiki kinatarajiwa kufikia 1,500–2,000 kWh kwa mwaka, kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya viwanda vidogo, magari ya umeme, majokofu, kompyuta, na vifaa vya kisasa vya nyumbani. Hii inaendana na mwelekeo wa taifa kuelekea uchumi wa viwanda na matumizi ya teknolojia bunifu.

Mwaka 2050, Tanzania inalenga kufikia matumizi ya zaidi ya 3,000 kWh kwa mwaka kwa mtu mmoja, kiwango kinacholingana na maisha ya kisasa yenye vifaa vya umeme vya nyumbani, huduma bora za afya na elimu, na uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu. Hii inaashiria kuwa kila Mtanzania atakuwa na uwezo wa kutumia umeme kwa shughuli za uzalishaji, matumizi ya nyumbani, na huduma za kijamii kwa ufanisi mkubwa. Kwa ujumla, ongezeko hili la matumizi linategemea utekelezaji wa miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme kama Bwawa la Nyerere (2,115 MW), gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi, na vyanzo mbadala kama jua na upepo kutoka Singida, Njombe na Dodoma.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Msemwa alisisitiza kwa kauli yenye msukumo: “Maono lazima yawe makubwa kiasi cha kukutisha. Usipotishwa na ndoto zako, bora usipange kuota.” Kauli hii inabeba uzito wa dhamira ya taifa kuwekeza katika nishati ya umeme kwa kiwango ambacho si tu kinabadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja, bali kinaunda Tanzania mpya ya viwanda, ya TEHAMA, na ya huduma za kisasa. Dira ya Taifa 2050 si ndoto ya kawaida; ni ndoto kubwa ya Taifa linaloamua kuamka na kutembea kwa kasi ya umeme

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img