RAIS SAMIA AAHIDI UMEME MARA TATU YA SASA IFIKAPO 2030

Published:

Mgombea Urais kupitia chama cha Mapinduzi CCM Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani yake amesema kuwa, Tanzania itaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi wote ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi, kuboresha maisha ya wananchi na kuharakisha maendeleo ya viwanda. Kwa mujibu wa mpango ahadi za utekelezaji wa sekta ya nishati, matumizi ya umeme kwa mtu yanatarajiwa kuongezeka kutoka wastani wa kilowati-saa 103 kwa mwaka 2024 hadi 300 kWh mwaka 2030.

Ili kufanikisha lengo hilo, Rais Samia amepanga kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Megawati 3,077.96 mwaka 2024 hadi Megawati 8,000 mwaka 2030. Vilevile, mtandao wa usafirishaji wa umeme utaongezeka kutoka kilomita 7,745.4 hadi kilomita 13,366.85, sawa na ongezeko la kilomita 5,621.45, ambalo ni ongezeko la asilimia 72.6. Aidha, kiwango cha upotevu wa umeme kitapunguzwa kutoka asilimia 16 mwaka 2024 hadi asilimia 10 mwaka 2030, ikiwa ni punguzo la asilimia 37.5, kwa kutumia teknolojia bora na miundombinu ya kisasa.

Katika hatua nyingine, Serikali imejipanga kukamilisha usambazaji wa umeme kwa kuunganisha vitongoji 31,532 vilivyosalia, ambavyo ni sawa na asilimia 49 ya maeneo ya Tanzania Bara, pamoja na kaya na taasisi mbalimbali. Kupitia ushirikiano na sekta binafsi, huduma za umeme zitaendelea kufikishwa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa, kwa kutumia teknolojia mbadala na suluhisho bunifu. Serikali pia itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama vile jua, upepo na mawimbi ya bahari, ili kupanua vyanzo vya uzalishaji wa umeme na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya kawaida. Ili kuvutia uwekezaji, mfumo mpya wa kisera na kisheria utawekwa ili kuruhusu ushiriki wa sekta binafsi katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Katika kuhakikisha Watanzania wanapata nishati salama ya kupikia, Serikali inalenga kuhakikisha angalau asilimia 50 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2030. Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha matumizi na uwekezaji wa nishati safi, kupunguza gharama za vifaa na majiko sanifu, pamoja na kuongeza tafiti na ubunifu wa teknolojia husika. Mpango huu wa kina unadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nishati salama, nafuu na endelevu inapatikana kwa Watanzania wote.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img