Katika ahadi zake ndani ya siku 100, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,
imependekeza mpango wa kugharamia kwa asilimia 100 matibabu na
vipimo vya kibingwa kwa wananchi wa kipato cha chini. Mpango huu
unalenga magonjwa yasiyoambukizwa yenye gharama kubwa kama vile
saratani, figo, moyo, kisukari, mifupa na mishipa ya fahamu ambayo
yamekuwa kikwazo kwa wananchi wengi kumudu huduma za matibabu.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025, Tanzania inakadiriwa kuwa na
jumla ya watu milioni 65, ambapo takriban asilimia 26.4 ya wananchi hao
sawa na watu milioni 17.16 wanatajwa na Benki ya Dunia kuwa wanaishi
chini ya kiwango cha umasikini wa kipato na hawa ndio wananchi
wanaolengwa moja kwa moja na Rais Samia kupitia mpango huu wa
huduma za afya bila malipo, kama sehemu ya ajenda ya kuimarisha usawa
wa kijamii na haki ya msingi ya kupata matibabu kwa kila Mtanzania.

