UDSM WAAZIMIA KUSIMAMA NA RAIS SAMIA

Published:

Prof. Alexandra Makulilo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akiwa na Bw. David Kafulila, Mkurugenzi wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), wakielekea kwenye Kongamano la kujadili mwenendo wa uchumi chini ya Awamu ya Sita.

Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere UDSM kwa sauti moja waliunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hii ni kufuatia tamko lao ambalo pamoja na mambo mengine walisema mwenendo wa Uchumi chini ya Awamu ya Sita ni wakuridhisha sana japo juhudi zaidi zinapashwa kuwekwa PPP kuelekea Dira 2050, Kongamano hili liliwakutanisha wasomi na watunga sera akiwamo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Mhe Majaliwa Khassimu Majaliwa.

Mjadala huo ulisisitiza pia diplomasia ya uchumi kama kichocheo cha biashara na uwekezaji, umuhimu wa PPP katika miundombinu ili kupunguza mzigo kwa serikali, na ushiriki wa Sekta binafsi katika kukuza rasilimali watu. Hata hivyo, Ujumbe mkuu ulikuwa ni kuunga mkono Dira2050 iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kutoa wito wa kuimarisha ushindani wa soko, kuendeleza PPP, na kuwekeza kwenye ujuzi na teknolojia. Kongamano hili limejenga daraja kati ya taaluma na utekelezaji wa sera kwa ajili ya uchumi jumuishi na imara.

HAYA NI BAADHI YA MAAZIMIO YA KONGAMANO HILO WAKIWEMO WANAUDASA.

“Washiriki wanaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza diplomasia ya uchumi kupitia Sera Mpya ya Mambo ya Nje. Wanaona uzinduzi wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ni kichocheo cha biashara ya kimataifa na uwekezaji katika nguvukazi kuelekea Dira 2050. Hata hivyo, wanashauri kuimarisha mazingira ya ushindani ili Tanzania inufaike zaidi na fursa za kikanda na kimataifa kwa maendeleo ya wananchi.”

Aidha, wamesisitiza:

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya ujenzi mkubwa wa miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, barabara, bandari na umeme. Hata hivyo, tunashauri kuimarishwa kwa uwekezaji kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kwa kuwa hatua hii itapunguza mzigo wa kifedha kwa serikali na kuruhusu rasilimali zaidi kuelekezwa kwenye maeneo muhimu ya kukuza rasilimali watu, ikiwemo elimu na afya kwa lengo la kuchochea uchumi jumuishi.”

SOMA HAPA CHINI HAYA MAAZIMIA YA KONGAMANO HILI

👇🏿

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
KIGODA CHA UPROFESA CHA MWALIMU J.K NYERERE KATIKA TAALUMA ZA UMAJUMUI WA AFRIKAKWA USHIRIKIANO NA KITUO CHA UBIA KATI YA SEKTA YA UMMA NA SEKTA BINAFSI (PPPC)

Nguvukazi yenye Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa: Kuendeleza Urithi wa Mwalimu Nyerere kuelekea Dira 2050

MAJUMUISHO YA KONGAMANO

Ndugu Washiriki wa Kongamano, kwa ruhusa yenu, napenda kuwaletea majumuisho yanayotokana na mawasilisho, mijadala, na michango yenu katika Kongamano hili:-

  1. Mwalimu Julius Nyerere aliamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na wananchi wenye ujuzi, maadili, uzalendo na bidii ya kazi. Hivyo, nguvukazi ni rasilimali kuu ya maendeleo. Maono, fikra na falsa za Mwalimu Nyerere juu ya maendeleo zinaendelea kuongoza sera na mikakati ya taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.
  2. Kujenga Uchumi mkubwa duniani kote hutekelezwa kupitia ushirikiano na sekta binafsi yenye nguvu. Vivyo hivyo, ndoto kuu zilizoainishwa katika Dira 2050 zitatimia kupitia ushiriki mpana wa sekta binafsi. Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni nyenzo muhimu katika kufanikisha kujenga Uchumi mkubwa na jumuishi. Uchumi mkubwa na jumuishi ni msingi wa uwekezaji katika kuendeleza nguvukazi ya taifa. Hivyo basi ubia yaani “PPP” upewe msukumo wa kutosha ili kuleta matokeo makubwa nchini.
  3. Elimu ina nafasi kubwa katika kukuza nguvukazi kuelekea dira ya 2050. Washiriki wanatambua juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza kwenye elimu ili kuimarisha nguvukazi ya taifa. Hata hivyo, wanasisitiza msukumo zaidi uelekezwe kwenye matumizi ya teknolojia, mafunzo kwa vitendo, na ujasiriamali ili kuunda nguvukazi yenye ushindani na uwezo wa kujiajiri. Pia, wanasisitiza umuhimu wa kuboresha mitaala na miundombinu ya elimu ili iendane na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya taifa.
  4. Washiriki wanaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza diplomasia ya uchumi kupitia Sera Mpya ya Mambo ya Nje. Wanaona uzinduzi wa Sera Mpya ya Mambo ya nje ni kichocheo cha biashara ya kimataifa na uwekezaji katika nguvukazi kuelekea Dira 2050. Hata hivyo, wanashauri kuimarisha mazingira ya ushindani ili Tanzania inufaike zaidi na fursa za kikanda na kimataifa kwa maendeleo ya wananchi.
  5. Katika uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya 2050 tarehe 17 Julai 2025, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisisitiza wajibu mkubwa wa wanazuoni na wanataaluma katika kuendesha mageuzi ya kisera, kisheria, kitaasisi, kiutaalamu na kifikra kuelekea utekelezaji wa dira hiyo. Hivyo basi, wanazuoni kupitia tafiti, ubunifu, ufundishaji, usambazaji wa maarifa na mijadala endelevu, ni chachu ya mabadiliko ya msingi yanayolenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa taifa.
  6. Mijadala ya kitaaluma ni kichocheo muhimu cha kuibua fikra tunduizi na mbinu bunifu za kutatua changamoto zinazokabili taifa katika safari ya maendeleo.
  7. Wadau wanakubaliana kuwa utekelezaji wa Dira ya 2050 unategemea wananchi kuendeleza Umoja, Amani na Utulivu— misingi iliyojengwa na Mwalimu Nyerere. Kwa kuhimiza mshikamano wa kitaifa, Nyerere alitufundisha kuishi kwa amani na kushirikiana kwa maendeleo. Wadau wanasisitiza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda misingi hii kama nguzo muhimu ya mafanikio ya Dira 2050.

Hivyo basi, kwakuzingatia yaliyojadiliwa, Kongamano linaazimia yafuatayo:-

i. Urithi wa Mwalimu Nyerere kupitia maono, fikra na falsafa yake viendelee kuwa msingi muhimu wa sera na mikakati ya maendeleo nchini Tanzania katika safari kuelekea Dira ya Maendeleo ya 2050.

ii. Kujenga nguvukazi, Serikali ikishirikiana na wadau iendelee kuwekeza katika watu, kuhamasisha bidii na ubunifu, na kudumisha maadili ya kazi, ili taifa liweze kufikia maendeleo endelevu na shirikishi, na hivyo kutimiza malengo ya Dira ya 2050.

iii. Serikali iendelee kuboresha na kuweka mazingira wezeshi kwa vyuo vikuu katika utafiti, ubunifu, na kuwa chemichemi ya mawazo na mijadala ya kitaifa, ili viweze kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza nguvukazi ya taifa kwa ajili ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050.

iv. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya ujenzi mkubwa wa miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, barabara, bandari na umeme. Hili ni jambo la msingi na kupongeza. Hata hivyo tunashauri kuimarishwa kwa uwekezaji kupitia ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP). Hatua hii itapunguza mzigo wa kifedha kwa serikali na kuruhusu rasilimali zaidi kuelekezwa maeneo mengine muhimu ya kukuza rasilimali watu, ikiwemo elimu na afya kwa lengo la kuchochea kukua kwa Uchumi jumuishi.

v. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa kukuza rasilimali watu. Hata hivyo kujenga nguvukazi yenye ujuzi mkubwa ipo haja ya kupanua nafasi ya ushiriki wa sekta binafsi ili kuongeza ufanisi, uvumbuzi, na wigo wa fursa zitakazochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo kutengeneza Uchumi jumuishi.

vi. Serikali ianzishe Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji na Ujuzi utakaowezesha kuendeleza rasilimali watu, hususan vijana, kwa kutoa mafunzo, mitaji, na fursa za ubunifu na ajira. Aidha, ianzishwe kanzidata ya kitaifa ya vijana wenye ujuzi ili kutambua, kuunganisha na kuwaweka wazi katika soko la ajira la ndani na kimataifa. Hatua hizi zitasaidia kujenga nguvukazi shindani, jumuishi na yenye mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050.

vii. Wananchi waendelee kukuza na kudumisha umoja, amani, mshikamano na maadili kama msingi wa maendeleo ya taifa, sambamba na kuhuishi urithi wa Mwalimu Nyerere.

11 Oktoba 2025
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Dar es Salaam

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img